Friday, October 11, 2013


DAR ES SALAAM
Watu wawili wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya utapeli , huku mmoja akitumia kitambulisho kinachomtambulisha kuwa ni ofisa mwandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa, wametiwa mbaroni jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo ambalo liligusa hisia za watu wengine lilitokea juzi maeneo ya Kawe, wakiwa katika Hoteli ya Picol Beach saa 2.30 siku baada ya kuwekewa mtego.

Watuhumiwa hao watanashati waliokamatwa katika tukio hilo wametambuliwa kuwa ni Fadhili Hamisi Mafutari ambaye anadaiwa kutumia kitambulisho cha Idara ya Usalama wa Taifa, kikiwa na jina la Kennedy Magige na picha yake.

Pia anatumia simu yenye namba 0654-084-445 iliyosajiliwa kwa jina la Kennedy Magige, ingawa rafiki yake ambaye amekamatwa naye kwenye tukio hilo, Tabula Abdallah Mayenga, alisema anamfahamu na jina lake, Fadhili Hamisi Mafutari.
Watu hao walikamatwa baada ya kuwekewa mtego na watu wanaodai kutapeliwa na Mayenga katika tukio lililotokea Ijumaa, wiki iliyopita maeneo ya Maua Resort Beach.

Akisimulia tukio hilo, mmoja wa mashuhuda alisema baada ya kutapeliwa, walianza kuweka mtego na kufanikiwa kumnasa Magige, kwa kutumia mtu mwingine aliyempigia simu na kujifanya ana shida naye.

Mtoa habari wetu huyo, alidai kwamba wakati Magige anawafanyia tukio hilo la utapeli, hakuwa anafahamu k ama wamebaki na namba yake simu na baada ya kufuatilia, walibaini imesajiliwa kwa jina la Magige.

Baada ya kufika, alitiwa mbaroni pamoja na mwenzake na kuanza kushushiwa kipigo kikali na wananchi wenye hasira, ambapo ilibainika anamiliki kitambulisho kinachomtambulisha kuwa ni ofisa mwandamizi Idara ya Usalama wa Taifa.

Lakini alipohojiwa, Magige alijitambulisha kuwa yeye ni mfanyabiashara wa mazao aina ya nafaka kauli ambayo ilitofautiana na rafiki yake ambaye alikamatwa naye kwenye tukio hilo, kwani alisema Mafutari (Magige) ni mfanyabiashara wa magari.

Mayenga alisema yeye ni fundi seremala na kwamba alifika hotelini hapo kufuata hela kidogo kwa rafiki yake,lakini ghafla aliona watu wanaanza kumfuatilia na hakuwa na njia ya kukimbia kwani alihisi ataitiwa mwizi.

No comments:

Post a Comment